SIKU moja baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya ya mafuta, kumejitokeza uhaba mkubwa wa petroli nchini, hasa katika jiji la Dar es Salaam ambako lita moja jana ilifika Sh3,000 kwa bei ya ulanguzi.
Uhaba huo wa petroli umesababisha ulanguzi mkubwa wa bidhaa hiyo katika kona mbalimbali za jiji la Dar es Salaam, huku wilaya ya Kinondoni ikionekana kuathirika zaidi kutokana na kukosa kabisa petroli.
Misururu ya watu wakiwa na madumu mikononi ilionekana katika vituo mbalimbali vya mafuta kuanzia pembezoni hadi kati kati ya jiji la Dares Salaam, huku mamia ya magari yakiwa kwenye foleni kusuburi mafuta kwenye vituo vichache vilivyokuwa vikiuza bidhaa hiyo.
Utaratibu wa kuyafuata mafuta hayo maeneo ya mbali na kuyapeleka maeneo ambayo hakuna kabisa, ndio uliofanya nishati hiyo iuzwe kwa bei ya ulanguzi.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara waliliambia MIWANI BLOG kwamba kuadimika kwa petroli jana, kulitokana na mgomo baridi uliofanywa na wafanyabiashara wa nishati hiyo kupinga uamuzi wa Ewura kushusha bei ya petroli kutoka Sh1,990 hadi Sh1,882.
Katika bei hiyo mpya, dizeli sasa inauzwa kwa Sh1,976 badala ya Sh2,075 na mafuta ya Taa Sh1,958 kutoka 2,049 .
Lakini, vyanzo vingine vililiambia MIWAN BLOG kwamba tatizo hilo limetokana na bohari za mafuta kushindwa kutoa huduma siku ya Jumamosi na Jumapili.
Kauli ya Ewura
Meneja Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo alikiri kuwapo kwa tatizo hilo na kuthibitisha kuwa limetokana na tangazo lake la kushusha bei ya mafuta.
"Tunajua hali hiyo kwamba ni ngumu na kama mamlaka, tunaendelea kulifanyia kazi suala hilo. Tutahakikisha kuwa tunalipatia ufumbuzi (tatizo) haraka iwezekanavyo," alisema Kaguo na kufafanua:
"Kuanzia leo (jana) tumekuwa na bei mpya ya mafuata ambayo ikilinganishwa na bei ya juma lililopita, imeshuka kwa kama Sh100 hivi. Sasa nini kinatokea? Tuna watu wawili wanaofanya biashara ya mafuta; Coco na Dodo."
Aliendelea, "Coco ni kampuni kubwa zinazoingiza mafuta na kuyasambaza kwa Dodo ambao ni wafanyabiashara wadogo. Hawa wadogo sasa ndio wanaoona kwamba kuuza mafuta yao sasa kwa bei hii mpya ni hasara. Lakini tunalifanyia kazi suala hilo na kuanzia mchana (jana) au kesho (leo) hali itatengamaa."
Uchunguzi wa MIWANI BLOG
Uchunguzi umebaini kuwa uhaba huo wa mafuata umefanya waendesha pikipiki kuingia mitaani na kuanza kusaka mafuta ili kuweza kuyauza kwa bei kubwa ya Sh 2,800 hadi Sh3,000 kwa lita kukidhi mahitaji ya watumiaji wa bidhaa hiyo.
Vituo vilivyokuwa wazi vilikuwa vikiuza bei iliyopangwa na Ewura lakini upatikanaji wa bidhaa hiyo umekuwa wa shida hivyo, kutafsiriwa na watumiaji kuwa ni mgomo wa kutaka bei kupandishwa.
Baadhi ya maeneo katika vituo vya mafuta vimekuwa vikiuza diseli na mafuta ya taa huku petrol ikiwa imekwisha na kusema, wanafuatilia katika bohari kuweza kuindokana na tatizo hilo.
Walisema uhaba wa upatikanaji wa mafuta unaweza kuongezeka iwapo bohari zitashindwa kuruhusu usambazi wa mafuta wa haraka kwa wafanyabiashara kutokana na uhitaji mkubwa wa watumiaji petrol.
Vituo vinavyoonekana kutotoa huduma ya mafuta ya Petroli jijini ni BP ambao karibu vituo vyao haviuzi mafuta ya aina zote, petroli hata dizel.
Baadhi ya vituo vya Gapco kama kati kati ya jiji karibu na jengo la Holland vimekuwa vikiuza mafuta hadi jana jioni, lakini katika baadhi ya maeneo haviuzi.
Oilcom baadhi ya maeneo kama mtaa wa Nkrumah vinauza mafuta maeneo mengine haviuzi, Camel Oil baadhi vinauza baadhi havizuzi katika maeneo tofauti Big Bon vituo vyake vya Sinza na Msimbazi vimekuwa vikiuza mafuta.
Maeneo ya Mwenge Bamaga, Sayansi na Kijitonyama huduma za mafuta zilikuwa zikitolewa lakini huduma hiyo ilikuwa ya taratibu sana kiasi cha kusababisha misururu mirefu ya magari na watu.
No comments:
Post a Comment