Monday, 19 December 2011

CHADEMA WAMKARIBISHA, CCM WAPONDA KUFUKUZANA

CHADEMA WAMKARIBISHA, CCM WAPONDA KUFUKUZANA
Waandishi Wetu wa MIWANI BLOG 


MSAJILI wa Vyama vya Siasa Nchini, John Tendwa amemkingia kifua Mbunge wa Kigoma Kusini kupitia NCCR Mageuzi, David Kafulila ambaye alifukuzwa uanachama na Halmashauri Kuu ya chama hicho mwishoni mwa wiki iliyopita.

Badala yake Tendwa katika kauli yake jana alivitaka vyama vya siasa kutumia busara katika kutatua migogoro yake na siyo kutoa uamuzi wa kukomoana kama ya kumfukuza mtu uanachama.

“Kila mara nasema kwamba, vyama viwe makini panapotokea migogoro. Wafanye majadiliano kupitia vikao na sio kuchukua uamuzi wa haraka kufukuzana uananchama,”  alisisitiza Tendwa.  Tendwa alisema hayo jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano wa  Mafunzo ya viongozi wa Baraza la vyama vya Siasa nchini. Mafunzo hayo yalihusu uongozi, uwajibikaji na utawala bora.  Kauli hiyo ya Tendwa imekuja siku tatu tangu Chama cha NCCR-Mageuzi kimfukuze uanachama Kafulila kwa madai ya kukiuka taratibu za chama hicho.

“Mimi kama Msajili siingilii mamlaka ya chama chochote na sina mamlaka ya kikatiba kufanya hivyo. Lakini, katiba haimruhusu (Kafulila) kuendelea na uongozi (mbunge) hadi awe na chama, hivyo kunatakiwa sasa, kuandaliwe uchaguzi mdogo,”alisema Tendwa na kuongeza:  "Kuandaa uchaguzi mdogo ni gharama kubwa. Uchaguzi mmoja gharama yake ni zaidi ya Sh19 bilioni. Kwa suala kama hili tujiulize nani amesababisha gharama, tusiishie tu kuupigia kelele ufisadi, tuangalie na sisi viongozi wa vyama tunaisaidia vipi serikali?”

Alisema unapoitishwa uchaguzi lazima kuwaandaa wasimamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kusimamia uchaguzi, polisi kwa ajili ya usalama na mahitaji mengine na kwamba fedha zinazotumika zingeweza kugharamia shughuli nyingine za maendeleo.  Alitoa mfano wa uchaguzi mdogo wa Igunga ambao alisema walioshiriki wanafahamu gharama na usumbufu walioupata.

 Hata hivyo Tendwa alisema, Kafulila bado ana nafasi ya kukata rufaa ndani ya chama chake na hata nje ya chama. Alifafanua: “Ana uhuru kwenda mahakamani na akishinda ataendelea kuwa mbunge".

 Alifafanua kwamba mbunge huyo ana haki ya kwenda mahakamani kukata rufaa na kwamba makahama ikiona alikiuka sheria na taratibu za chama basi hapo lazima uchaguzi mdogo ufanyike  na serikali italazimika kuingia gharama kubwa.

Awali, akizungumza katika mkutano huo uliohusisha viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa, Tendwa alisema matatizo yanayotokea ndani ya taasisi, asasi na hata kwenye vyama vya siasa yanatokana na mawasiliano hafifu hivyo viongozi bora wanatakiwa wawe na uwezo wa kuwasiliana.  “Kama kiongozi anatakiwa kutoa onyo au karipio kwa mtumishi ama mtendaji ni vizuri na busara kutoa onyo hilo bila kuonyesha hisia za chuki binafsi,”alisema Tendwa.

 Alisema migongano mingi inatokana na udhahifu katika kuainisha ukomo wa madaraka na kwamba busara inatakiwa itumike kutambua yale kiongozi anayotakiwa kuamua na yale ambayo lazima apate ushauri kabla ya kutoa uamuzi wake.

 Matumaini ya Kafulila
Kwa upande wake Kafulila alisema hawezi kuzungumza kwa undani  kuhusu hatma yake kisiasa na kusisitiza kwamba, jambo hilo litakwisha.  Akizungumza Dar es Salaam jana Kafulila alisema, ''Kuna taratibu zinaendelea ndani ya chama, kwa sasa sitaweza kuzungumza lolote, kila jambo liko ndani ya chama (NCCR Mageuzi) na taratibu zinaendelea".  Alipoulizwa taarifa kwamba anataka kufungua kesi ya kikatiba kupinga uamuzi wa chama hicho kumfukuza uanachama alisema, ''Unajua nini kuna…, kuna mambo yanaendelea hivyo siwezi kuzungumza kwa sasa, ila ninachopenda kuwaeleza watanzania ni kwamba hili jambo litakwisha tu,''.

Hawezi kukata rufaa
Mwanasheria wa NCCR Mageuzi, Dk Sengondo Mvungi alisema Kafulila hawezi kukata rufaa sehemu yoyote dhidi ya uamuzi wa kumfukuza uanachama kwa mujibu wa kanuni ya 7 (2) ya chama hicho.

Kanuni hiyo ya 7(2) ya nidhamu na usuluhishi sehemu ya (d) inaeleza kuwa, baada ya uamuzi wa mwisho kufanywa, kikao husika kitatoa maelekezo kwa kikao au vikao vya chini vyenye mamlaka ya kuchukua hatua au kutoa adhabu kwa kiongozi au mwanachama husika.  Kipengele (f) kinasema uamuzi utakaofanywa kwa mujibu wa kupengele (d) utakuwa wa mwisho ila tu pale unapomhusu Mwenyekiti Taifa na Makamu Mwenyekiti (Zanzibar) ambao uamuzi wa mwisho kuwahusu wao ni Mkutano Mkuu.
Kanuni hiyo hiyo sehemu ya 7(1) inaeleza, ‘'Mlalamikiwa au mhusika atakuwa na haki ya kukata rufaa kwenda kamati ya nidhamu na usuluhishi iliyo katika kikao cha ngazi ya juu zaidi ya kikao husika, na kamati hiyo itakuwa na uwezo sawa na ule wa kamati ya kwanza, ila tu haitapokea ushahidi mara ya pili'’.  Hata hivyo, kwa mujibu wa Ibara ya 10(4) ya Katiba ya chama hicho, ‘'Mwanachama ana haki ya kujitetea mbele ya kikao cha chama kinachohusika katika mashitaka au madai yoyoye, na kuwa na haki ya kukata rufaa kwenye vikao vya juu iwapo mhusika hakuridhika na uamuzi wa kikao cha chini.’’

Chadema wamkaribisha Kafulila
Wakati hayo yakiendelea, Chadema kimemkaribisha mbunge huyo kujiunga na chama hicho baada ya kufukuzwa NCCR-Mageuzi.  Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa Facebook alisema: “Kafulila akumbuke kwamba hakufukuzwa Chadema ila alijiondoa mwenyewe”.
"Milango yetu ipo wazi kwa mujibu wa Katiba, Kanuni na taratibu za chama chetu,"alisema  Zitto.  Hata hivyo,  Zitto ameeleza kuwa anaamini NCCR Mageuzi watamaliza matatizo yao kwa mujibu wa katiba ya chama chao na  Kafulila atazikabili changamoto hizo kama kiongozi kijana wa kisiasa badala ya kukata tamaa.
"Ifahamike wazi kabisa kwamba David ni mtu huru mwenye mawazo yake na maamuzi yake. Kwamba sisi ni marafiki wa karibu na kwamba tunatoka mkoa mmoja,"alisema na kukanusha taarifa zinazomuhusisha yeye na Kafulila kuhusu mgogoro ndani ya NCCR Mageuzi.

"Napenda kuweka wazi kwamba sihusiki kwa namna yeyote ile na migogoro ya chama kile. Ninaomba nisihusishwe na mambo yasiyonihusu. Ni dhahiri kwamba kuvuliwa uanachama kwa David ni jaribio kubwa kwa mfumo wetu wa demokrasia kama ilivyokuwa huko nyuma wakati kina Erasto Tumbo walipovuliwa uanachama wa chama chao cha UDP."
Zitto alisema haina maana kwamba lolote afanyalo ama Kafulila amemtuma yeye  au anahusika na kuongeza kwamba,  anaheshimu msimamo wake siku zote na huwa yupo upande wa anayeonewa, kudhulumiwa na mnyonge.   "Msimamo huu wa msingi usiwape watu nafasi ya kunihusisha na mambo ya chama dhaifu kisicho na dira kama NCCR-Mageuzi,"alisema.

Nape abeza Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye  alisema vijana kwenye vyama vya siasa wanatakiwa washauriwe na kupewa maonyo badala ya kufukuzwa.  Nape ambaye aliwahi kuingia kwenye malumbano na wazee ndani ya CCM akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu Yusuph Makamba, hadi kufikia hatua ya kumwambia kijana huyo, “alifungiwa duniani hadi mbinguni”,  alisema vijana waelimishwe.


Alifafanua kwamba hata enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere watu walikuwa wanakosea na wanaelimishwa na kwamba kama Nyerere angekwua na hasira hizo hata wanasiasa wanaoonekana leo wasingekuwepo.

Nape alivitaka vyama vya siasa vijenge utamaduni wa kuvumiliana na kuwalea vijana kwa kuwafundisha, badala ya kuwafukuza uanachama.  “Mimi sio muumini wa kufukuza wana siasa vijana lakini kama tukiendelea hivi mwisho wa siku tutateketeza wanasiasa;  “Kasi ya wanasiasa vijana ni kubwa lakini inawezekana kasi hii imeanza kuwatia homa wanasiasa wa zamani hasa kama mfano huu wa Kafulila,”alisema.
Alisema pia kama kutafanyika uchaguzi mdogo katika jimbo hilo wanaamini watashinda na kwamba anawashukuru NCCR, kwa kuwarejeshea jimbo hilo.    

No comments:

Post a Comment