Sunday, 15 January 2012

Hoyce Temu alamba nondoozz


hoyce temu alamba nondoozz!



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Benard Membe akimtunukia Afisa Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa ambaye amewahi kuwa Miss Tanzania 1999 na Mwandishi wa kitabu NAYAKUMBUKA YOTE Hoyce Temu Stashahada ya Uzamili katika Menejimenti ya Mahusiano ya Kimataifa (Post Graduate Diploma in Management of Foreign Relations) katika Mahafali ya Kumi na Sita ya Chuo cha Diplomasia jijini Dar es Salaam.

Paul Scholes amefunga bao lake la kwanza baada ya 
kurejea tena kuichezea Manchester United ambayo 
imesogea na kuwa na pointi sawa na Manchester City 
baada ya kuilaza Bolton mabao 3-0.

Mkongwe Paul Scholes aifungia Man United bao la kwanza
Mkongwe Paul Scholes aifungia Man United bao
la kwanza
Lakini Scholes, ambaye sasa amefika umri wa miaka 37, alifanikiwa kupachika bao sekunde chache kabla mapumziko baada ya kuunganisha pasi ya pembeni ya Rooney.United ilipoteza nafasi nyingi za kufunga kipindi cha kwanza lakini kazi nzuri aliyoifanya mlinda mlango wa Bolton Adam Bogdan iliisaidia Bolton kuepuka kipigo kikali zaidi. Alifanikiwa kuokoa mkwaju wa penalti uliopigwa na Wayne Rooney katika kipindi cha kwanza.
Bolton ilionekana kuimarika kipindi cha pili na Manchester United walionekana kusinzia kidogo, lakini alikuwa Danny Welbeck aliyeizindua tena Man United kwa kupachika bao la pili kabla ya Michael Carrick kufumua mkwaju wa umbali wa yadi 20 na kuandika bao la tatu.
Matokeo hayo yameonekana kuipa faraja Man United baada ya kupoteza michezo miwili ya Ligi Kuu ya England, pia kuzidi kuipa changamoto mahasimu wao Man City ambao siku ya Jumatatu watasafiri hadi Wigan kuikabili timu hiyo.
Bao pekee alilofunga Frank Lampard mapema katika kipindi cha kwanza, limeiwezesha Chelsea kuipunguzia kasi Sunderland iliyoanza kucharuka baada ya kumpata meneja mpya Martin O'Neill.
Lampard alitumia uamuzi wa haraka kuuwahi mpira na kupachika bao kwa mkwaju wa karibu baada ya fataki aliyoachia Fernando Torres kugonga mwamba na kurejea uwanjani.
Torres, Lampard na Juan Mata wote walikosa nafasi nzuri za kufunga kipindi cha kwanza.
Lakini Sunderland walipata nafasi nyingi kipindi cha kwanza na walikosa nafasi muhimu ya kupachika bao dakika za mwisho ambapo Craig Gardner na Nicklas Bendtner walishindwa kufunga.
Blackburn waliweza kuhimili vishindo licha ya mfungaji wao mashuhuri Yakubu kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika za mwanzo na kutoka eneo la hatari la kushuka daraja kwa mara ya kwanza tangu mwezi wa Septemba kwa ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Fulham.
Mshambuliaji Yakubu alioneshwa kadi nyekundu kipindi cha kwanza baada ya kumfanyia rafu mbaya Danny Murphy.
Lakini wakicheza nyumbani Blacburn walifanikiwa kupata bao la kwanza lililofungwa na Morten Gamst Pedersen kwa mkwaju wa adhabu ya moja kwa moja kabla ya David Dunn kupachika bao la pili.
Damien Duff aliipatia Fulham bao la kufutia machozi, kabla ya Mauro Formica kuikamilishia kazi Blackburn kwa kuandika bao maridadi la tatu.
Victor Anichebe akiingia mchezaji wa akiba alifanikiwa kuipatia Everton pointi moja baada ya Aston Villa kuonesha kandanda ya ovyo wakicheza uwanja wa nyumbani.
Darren Bent aliipatia Aston Villa bao la kwanza baada ya kupokea pasi ya Stephen Ireland katika dakika ya 56.
Meneja wa Everton David Moyes aliona hakuna cha kuikomboa timu hiyo bila ya kumuingiza Anichebe ambaye alifanikiwa kuisawazishia Everton baada ya Landon Donovan kumchezesha kwa pasi murua.
Robbie Keane aliingia kipindi cha pili kwa Villa ikiwa ni mchezo wake wa kwanza tangu ajiunge na timu hiyo kwa mkataba wa muda mfupi, lakini hakuweza kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi.
Bao la kichwa la dakika za mwisho lililofungwa na Steve Morison liliisaidia Norwich kushinda kwa kuilaza West Brom mabao 2-1.
Mkwaju wa juu wa Andrew Surman uliiwezesha Norwich kuandika bao la kwanza muda mfupi kabla ya mapumziko wakati West Brom wakionekana kukosa nafasi nyingi za wazi kupachika mabao.
Shane Long alizinduka haraka na kuipatia bao West Brom kwa kwaju wa penalti baada ya Jerome Thomas kuchezewa rafu.
Lakini Morison aliangushia kipigo cha nne mfululizo West Brom kwa kuandika bao la pili.
Liverpool imekosa nafasi ya kuingia katika timu tano bora za juu baada ya kubanwa na Stoke na kuandika sare ya saba kwa michezo iliyocheza uwanja wa nyumbani wa Anfield.
Dirk Kuyt alipoteza nafasi nzuri ya kuipatia bao Liverpool wakati mpira wake wa kichwa ulipotoka nje.
Martin Skrtel alidonyoa mpira wa kichwa dakika za mwisho lakini Liverpool walikuwa wamejipanga zaidi kwa kuachia mikwaju ya mbali ambayo haikuzaa matunda.
Mkwaju alioupiga Matthew Etherington kwa kumlenga mlinda mlango wa Liverpool Jose Reina ulikuwa ni moja ya majaribio machache ambayo Stoke iliyafanya. Hadi mwisho timu hizo hazikufungana.
Tottenham nayo ilikosa nafasi nyeupe ya kufikisha pointi sawa na vinara wa ligi baada ya kubanwa na kutoka sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Wolves.
Steven Fletcher alikuwa wa kwanza kuipatia Wolves bao kwa mkwaju wa karibu baada ya mlinda mlango Brad Friedel kupangua mpira wa kichwa uliopigwa na Roger Johnson.
Luka Modric aliisawazishia Spurs kwa mkwaju wa yadi 20 baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Gareth Bale ambaye alikosa kuuweka mpira wavuni na ukamkuta mfungaji ambaye hakufanya ajizi.
Wolves walijihami vizuri huku mlinda mlango Wayne Hennessey akiokoa michomo ya Aaron Lennon na Jermain Defoe.
Matumaini makubwa ya Tottenham yaliyoanza kuchomoza hivi karibuni ya kushinda ligi baada ya miaka 50 yalivurugika ambapo kama wangeshinda wangekuwa pointi sawa na Manchester zote mbili huko kileleni wakitenganishwa na wingi wa mabao.

Uchina yasema Marekani ni mchokozi


Gazeti la taifa la Uchina limechapisha makala yanayoishutumu Marekani kuwa "mchokozi", katika mvutano unaozidi Mashariki mwa Asia.
Jeshi la Marekani linataka ushirikiano na majirani wa Uchina
Katika taarifa ya ukurasa wa mbele, gazeti la People's Daily, la chama tawala cha Kikoministi cha Uchina, Adimeri Yang Yi anasema ni wazi kuwa mkakati mpya wa ulinzi wa Marekani, unazilenga Uchina na Iran.Makala hayo yanafuatia sera mpya ya ulinzi iliyotangazwa na Marekani, ambayo inasema italenga eneo la Asia.
Adimeri huyo anailaumu Marekani kwa matokeo ya miaka miwili iliyopita, ambayo amesema yanatishia usalama wa Asia.
Hakueleza matokeo yenyewe.
Aliongeza kusema kuwa ni wazi kuona nani ni mchokozi katika usalama wa eneo hilo.
Taarifa hiyo siyo ya serikali, lakini lazima ilipitishwa na serikali kuwekwa ukurasa wa mbele namna hivo.
Sera mpya ya Marekani iliyotangazwa juma hili, inasema mipango ya ulinzi ya Marekani sasa italenga Asia.
Kuna uwezekano wa kushirikiana na Uchina, lakini ilisema haijulikani wazi nini msimamo wa kijeshi wa Uchina.
Kwa hivo Marekani itahakikisha kuwa ina nguvu kuonesha masilahi yake Asia, na itazidisha maingiliano na washirika wake katika eneo hilo.

WATU 50 WAMEFARIKI KATIKA MLIPUKO WA BOMU - IRAQ


Wakuu wa Iraq wanasema mtu aliyejitolea mhanga ameripua bomu na kuuwa watu kama 50, katika shambulio dhidi ya mahujaji wa Kishia katika mji wa Basra, kusini mwa nchi.
Shambulio dhidi ya mahujaji wa Kishia, Iraq
Polisi walieleza kuwa mahujaji hao walikuwa wanaelekea msikiti mkubwa wa Washia nje ya Basra, mwisho wa ile wanayoita Arbain, moja kati ya vipindi vinavyoadhimishwa na Washia.
Inaarifiwa kuwa watu 90 wengine wamejeruhiwa.
Askari wa usalama 7 ni kati ya watu waliokufa.
Shambulio hilo linakuja wakati mvutano wa kisiasa unazidi baina ya Washia, walio wengi Iraq, na Wasunii.
Mwezi uliopita, serikali yenye Washia wengi, ilitoa amri ya kumkamata makamo wa rais aliye wa madhehebu ya Sunni, Tariq al-Hashemi, kwa mashtaka ya ugaidi.

MELI YA ZAMA WATU 40 BADO HAWAJAPATIKANA


Wakuu wa forodha wa Utaliana wanasema watu kama 40 bado wametoweka, baada ya meli ya abiria iliyobeba watu zaidi ya 4000 kwenda mrama katika mwambao wa Utaliana.
Meli ilizama Utaliana
 Msemaji wa walinzi wa pwani alieleza inawezekana kuwa watu wengine bado wako ndani ya meli.Shughuli za uokozi zimeendelea kutwa, huku wazamia mbizi wakipekua upande uliozama wa meli hiyo, Costa Concordia.
Abiria wawili kutoka Ufaransa na baharia mmoja kutoka Peru wanajulikana kuwa wamekufa.
Mkuu wa kampuni inayomiliki meli hiyo, Gianni Onorato, alisema ushahidi wa awali unaonesha kuwa meli iligonga mwamba;
nahodha haraka akafuata utaratibu wa kuwatoa abiria melini.
Lakini operesheni ilizuwilika kwa sababu meli yenyewe haraka ilipindukia ubavuni na kuzusha mtafaruku.
Taarifa za karibuni zinaeleza kuwa ofisi ya mashtaka ilimzuwia nahodha baada ya kumhoji.

MBUNGE REGIA ESTELATUS AFARIKI DUNIA


MBUNGE wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Regia Estelatus  Mtema (32), amefariki dunia baada ya gari alilokuwa akiendesha, kupinduka eneo la Mlandizi, Kibaha mkoani Pwani jana.

Ajali hiyo ilitokea saa 5:30 asubuhi karibu na Sekondari ya Ruvu, wakati mbunge huyo na watu wengine saba, wakisafiri kwa gari aina ya Toyota Landcruiser wakitoka Dar es Salaam kwenda Morogoro.Akielezea mazingira ya ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu, alisema mbunge huyo alifariki baada ya gari hilo alilokuwa akiendesha mwenyewe, kuacha njia na kupinduka.

Alisema ajali hiyo ilitokea baada ya Mtema kujaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake na ghafla aliona gari lingine likija kasi mbele yake,  katika kujaribu kulikwepa, ndipo gari hilo lilipinduka.

"Wakati akiwa hajalipita gari hilo aliliona gari lingine likija mbele kwa kasi , katika kulikwepa wasigongane uso kwa uso, alitoa gari lake barabarani na kusababisha kupinduka,’’ alisema Mangu.

Regia Mtema.Picha na Sanjito Msafiri na Maktaba
Alisema watu wengine saba  waliokuwa kwenye gari hilo walijeruhiwa, wawili kati yao  hali zao zilikuwa mbaya,  walipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dar es Salaam kwa matibabu zaidi, huku wengine watano, wakiwahishwa Hospitali Teule ya Tumbi Kibaha.

Aliwataja majeruhi waliolazwa Tumbi kuwa ni Lawrence Mtokambali (58), Benadetha Mtema (50), Peter Madesa (50) na Rogers Abdallah(18).

Chadema yatoa tamko
Chadema kilisema kuwa Mtema alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho na Waziri Kivuli wa Kazi na  alikuwa mchapa kazi hodari katika majukumu mbalimbali yakiwepo ya kijamii na kisiasa.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Chadema jana na kusainiwa na Katibu Mwenezi wa chama hicho, John Mnyika ilieleza kuwa viongozi wakuu wa chama hicho wakiongozwa na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Willibroad Slaa, wajumbe wa Kamati Kuu, Wakurugenzi wa chama hicho makao makuu na wabunge, wameshtushwa na kifo hicho na kuungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Chadema kimesema taarifa zaidi kuhusu taratibu za maziko, itatolewa mara baada ya kukamilisha majadiliano kati familia ya marehemu, chama na Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kufuatia kifo hicho, mkutano wa Chadema uliokuwa umepangwa kufanyika jana Mjini Kibaha umehirishwa hadi itakapotangazwa wakati mwingine.

Elimu yake
Mtema alizaliwa Aprili 21, 1980. Alisoma elimu ya msingi kati ya mwaka 1989 na 1995. Alijiunga na Shule ya Sekondari Forodhani, Dar es Salaam mwaka 1996 hadi  1999 na kuhitimu kidato cha nne.
Aliendelea kidato cha tano 2002 na sita kati ya mwaka 2000 na 2002 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Machame, mkoani Kilimanjaro.

Mwaka 2003 hadi 2006 alisoma Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na kupata Shahada ya Maarifa ya nyumbani na Lishe. Baada ya kuhitimu shahada yake, marehemu Mtema alifanya kazi katika taasisi mbalimbali kabla ya kujiunga na Chadema na kuteuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Vijana ya chama hicho.

Baadaye aliteuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Mafunzo ya chama hicho, nafasi ambayo aliishikilia hadi mwaka 2010 alipoteuliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum.

JK amtumia rambirambi Mbowe
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kufuatia kifo cha mbunge huyo.

Katika salamu hizo, Rais ameelezea kusikitishwa kwake na taarifa za kifo cha mbunge huyo na kueleza kwamba, marehemu Mtema  amepoteza maisha akiwa kijana na kwamba pigo hilo si kwa Chadema pekee bali kwa taifa zima.

“Nimepokea kwa masikitiko na huzuni nyingi habari za kifo cha Mheshimiwa Mtema katika ajali ya gari. Siyo kwamba ajali hii imechukua maisha ya kijana bali imelinyang’anya taifa mbunge hodari, na kwa hakika, kifo chake siyo tu ni pigo kwa chama chako bali ni pigo kwa sote na kwa taifa letu kwa jumla.

"Nakutumia wewe binafsi, chama chako na wanachama wake salamu za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo na msiba huu mkubwa," alisema Rais Kikwete kupitia taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.
Gari la Mbunge wa Viti Maalum wa Chadema, Regia Mtema alilopata nalo ajali iliyosababisha kifo chake jana, eneo la Ruvu, mkoani Pwani likiwa limeegeshwa katika Kituo cha Polisi cha Mlandinzi, mkoani humo.
Aliongeza: “Napenda ujue kuwa niko nanyi katika msiba huu. Napenda vilevile uniwasilishie salamu zangu za rambirambi za dhati kabisa kwa wana-familia, ndugu na jamaa wa marehemu Mheshimiwa Mtema.

Taarifa hiyo imemwomba Mbowe kufikisha salamu za Rais Kikwete kwa familia ya mbunge huyo na kuijulisha kuwa amepokea habari hizo kwa huzuni kubwa. "Wajulishe kuwa nawaombea kwa Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, awajalie uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu kwa sababu yote ni mapenzi yake.








Wananchi wamlilia


Katika kuonyesha kuguswa na kifo hicho mamia ya watu wanaotumia mtandao wa kijamii maarufu kwa jina la ‘Facebook’  walielezea kusikitishwa na kifo hicho huku wakitoa maoni mbalimbali.

 Miongoni mwa maelezo yao ni juu ya maneno aliyowahi kuyazungumza mbunge huyo kijana, ukiwamo ujumbe alioandika katika mtandao huo akiwataka wananchi wamweleze kero zao ili azifikishe katika mkutano ujao wa Bunge.

Ujumbe huo aliouandika Januari 10 mwaka huu na kuungwa mkono na watu 159 ulisomeka hivi;

“Wapenzi, habari zenu kama una kero yoyote unayoona inafaa ikasemewe bungeni au nje ya Bunge na Wabunge na Viongozi wa Chadema basi tupia hapa kero yako. Angalizo; isiwe kero binafsi..., karibuni sana pamoja tunaweza”.

Mtema anakuwa mbunge wa pili wa chama hicho kufariki dunia kwa ajali ya gari, Julai 27, 2008 Mbunge mwingine wa chama hicho Jimbo la  Tarime, Chacha Wangwe alikufa katika ajali ya gari

eneo la Pandambili mkoani Dodoma.

Taarifa ya Chadema ilieleza kwamba mipango ya mazishi ya marehemu inapangwa  nyumbani kwa baba yake, Tabata Dar es Salaam .